Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Januari 20, 2026 amefanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamadi Masauni, katika ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo Mlimwa jijini Dodoma.
Mazungumzo hayo yalilenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Muungano, ulinzi na uhifadhi wa mazingira pamoja na utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali katika maeneo hayo muhimu kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili pia namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Makamu wa Rais katika kusimamia masuala ya mazingira, hususan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Viongozi wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Dkt. Festo Dugange, pamoja na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Dkt. Richard Muyungi.
Mazungumzo hayo yamekuja ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa Serikali wa kufanya vikao vya ndani kwa lengo la kuimarisha uratibu wa shughuli za Serikali na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya wizara na taasisi unakwenda sambamba na malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya viongozi na taasisi zake katika kusimamia masuala ya Muungano na mazingira, kwa lengo la kuhakikisha maendeleo ya taifa yanapatikana bila kuathiri ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.


0 Comments