Halmashauri ya Jiji la Tanga, kupitia Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Bw. Simon Mdende, imetangaza kufunguliwa kwa zoezi la uombaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2025/2026, inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kiuchumi.
Mdende amesema Jiji la Tanga limetenga jumla ya shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kutolewa kwa vikundi vinavyokidhi vigezo kutoka makundi hayo maalum. Amesema tangazo la uombaji wa mikopo hiyo litadumu kwa muda wa siku 31.
Amefafanua kuwa baada ya kukamilika kwa kipindi cha uombaji, halmashauri itatumia takribani miezi miwili iliyobaki kufanya mchakato wa uhakiki na tathmini ya vikundi vilivyoomba, ikihusisha kamati mbalimbali zitakazotembelea vikundi husika kwa lengo la kuvihakiki na kuthibitisha taarifa zao.
Mndende amesema kuwa Halmashauri tayari imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya mikopo hiyo, na kusisitiza kuwa wajasiriamali watakaokidhi vigezo vyote vilivyowekwa ndio watakaonufaika na fursa hiyo muhimu ya kiuchumi.
Ameeleza kuwa mikopo hiyo inalenga makundi maalum ikiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuwawezesha kukuza na kuimarisha biashara zao ndogondogo na za kati.
Kwa mujibu wa Mndende, maandiko ya kuomba mkopo yanapaswa kuzingatia uhalisia wa biashara husika, mpango wa matumizi ya fedha pamoja na mkakati wa kurejesha mkopo kwa wakati ili kuhakikisha mzunguko wa fedha unaendelea.
Aidha, amewasisitiza waombaji kuhakikisha wanawasilisha maandiko yao kwa wakati na kufuata taratibu zote zilizowekwa, ikiwemo usajili halali wa vikundi au biashara zao katika mamlaka husika.
Mndende ameongeza kuwa Halmashauri itaendelea kutoa elimu na mafunzo kwa wajasiriamali ili kuwajengea uwezo wa kuandaa maandiko bora pamoja na kusimamia biashara zao kwa ufanisi zaidi.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kupunguza changamoto ya urejeshaji wa mikopo, ambayo imekuwa ikijitokeza kwa baadhi ya wanufaika wa awamu zilizopita.
Halmashauri ya Jiji la Tanga imekuwa ikitekeleza mpango wa mikopo ya asilimia 19 kama sehemu ya maagizo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha wananchi wanapata fursa za kujikwamua kiuchumi.
Kupitia mikopo hiyo, wajasiriamali wengi wamefanikiwa kupanua biashara zao, kuongeza ajira na kuchangia katika kukuza uchumi wa jiji la Tanga kwa ujumla.
Baadhi ya wajasiriamali waliopata mikopo hiyo katika awamu zilizopita wameipongeza Halmashauri kwa kuendelea kutoa fursa hiyo, huku wakishauri waombaji wapya kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa.
Halmashauri imewataka wajasiriamali wote wenye nia ya kuomba mikopo hiyo kufuatilia matangazo rasmi na kufika katika ofisi za Maendeleo ya Jamii ili kupata maelekezo zaidi kuhusu zoezi hilo.

0 Comments