WAZIRI WA FEDHA-BALOZI KHAMIS M.OMAR AAGIZA NIC KUANDAA MIKAKATI YA KUENDANA NA MALENGO YA MUDA MREFU YA NCHI

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameliagiza Shirika la Bima la Taifa (NIC) kuandaa mikakati madhubuti itakayoliwezesha kuendana na mwelekeo wa mipango ya muda mrefu ya nchi, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inaonesha fursa kubwa za ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya bima.

Mhe. Balozi Khamis ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu fursa za kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya bima.

Alisema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaonesha wazi fursa nyingi za kiuchumi, ambapo sekta ya bima imetajwa kuwa miongoni mwa sekta muhimu zitakazochangia kwa kiasi kikubwa katika kuchochea maendeleo ya taifa. Alisisitiza kuwa NIC, kama shirika la umma, linapaswa kujipanga mapema ili kunufaika na fursa zitokanazo na maendeleo ya viwanda, uanzishwaji wa kanda za viwanda na kanda maalum za kiuchumi, pamoja na sekta ya kilimo na nyinginezo.

“Tuna mipango mikubwa ya kitaifa. Tukiangalia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, kuna fursa nyingi za kiuchumi, ikiwemo katika sekta ya bima. NIC lazima ijipange sasa ili kuendana na kasi ya maendeleo hayo,” alisema Mhe. Balozi Khamis.

Aidha, aliagiza shirika hilo kujitangaza zaidi na kuongeza utoaji wa elimu ya bima kwa wananchi, ili waweze kuelewa umuhimu wa bima na kutambua fursa zilizopo, hususan katika kukabiliana na majanga mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge, alisema shirika hilo linaendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yake. Aliongeza kuwa NIC imejipanga kutoa huduma bora nchini kote na kuwekeza zaidi katika miradi ya maendeleo ikiwemo viwanda, miundombinu na masoko ya mitaji, kwa lengo la kuongeza mapato ya taifa.

Post a Comment

0 Comments