MKUU wa Msafara wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC–TZ), Brigedia Jenerali Baganchwera Rutambuka, amesema Bandari ya Tanga imeleta tija kubwa katika sekta ya usafirishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mikoa ya Kaskazini pamoja na nchi jirani.
Brigedia Jenerali Rutambuka ameyasema hayo baada ya wakufunzi, maafisa wanadhimu na washiriki wa Kozi ya Kumi na Nne ya chuo hicho waliopo mkoani Tanga kuitembelea bandari hiyo kwa lengo la kujionea ufanisi wa shughuli zake.
Amesema upanuzi wa bandari hiyo kwa kuongeza gati na kuboresha miundombinu umeongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi wa utoaji huduma, hali iliyopelekea kuongezeka kwa idadi ya meli zinazotia nanga, shehena za mizigo, mapato ya bandari pamoja na kupungua kwa muda wa kupakua mizigo.
Ameeleza kuwa Bandari ya Tanga ina nafasi ya kipekee ya kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji katika ukanda wa Kaskazini endapo maboresho yataendelea kufanyika.
Aidha, Brigedia Jenerali Rutambuka amesema mpango wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Bandari ya Tanga kuelekea ukanda wa Kaskazini na kuunganishwa na Korido ya Kati utachochea maendeleo ya kiuchumi kwa mkoa wa Tanga na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Operesheni wa Bandari ya Tanga, Bw. Gwakisa Mwaibuji, amesema mwaka 2018 Serikali iliwekeza shilingi bilioni 429.1 kwa ajili ya maboresho makubwa ya bandari hiyo.
Amesema kukamilika kwa maboresho hayo kumeongeza ufanisi wa operesheni, hali iliyopelekea kukua kwa uwezo wa bandari, kuongezeka kwa mapato pamoja na fursa za ajira.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Bandari ya Tanga ilihudumia zaidi ya tani milioni moja za mizigo, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya maboresho.
Mwaibuji amesisitiza kuwa Bandari ya Tanga inaendelea kushuhudia ongezeko la shehena kila mwaka na kila mwezi kutokana na mwitikio mkubwa wa wafanyabiashara wanaochagua kutumia bandari hiyo, hali inayoonesha imani kubwa waliyonayo katika huduma zinazotolewa.

0 Comments