Mabalozi wa Mashina ni Nguzo ya Kukipambania Chama – Dkt. Migiro

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha-Rose Migiro, amesema Mabalozi wa Mashina ni nguzo muhimu ya kukipambania Chama kwa kuwa ndiyo macho, masikio na daraja la kukiunganisha Chama na wananchi, sambamba na kulinda umoja kama nguvu ya kusonga mbele katika kuwatumikia wananchi.

Dkt. Migiro ameyasema hayo leo, Januari 20, 2026, jijini Dodoma wakati wa mkutano na Mabalozi wa Mashina wa Mkoa wa Dodoma. Amesema mashina ni ngome ya ulinzi wa Chama kwa kuwa yanaendelea kuwa walezi wa jamii, kuwaunganisha wananchi na kuhakikisha mshikamano unaimarika, akisisitiza kuwa siasa lazima iende sambamba na uchumi, jambo linalofanya mashina kuwa na tija kubwa kwa Chama.

Ameeleza kuwa mashina ni mahala sahihi pa kuikusanya jamii pamoja, kujadili masuala ya maendeleo na kutangaza kazi nzuri zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Aidha, amewataka Mabalozi wa Mashina kufanya vikao vya mara kwa mara na kuwasilisha maazimio yao katika ngazi za juu za Chama ili kupitia CCM waweze kuishauri Serikali iliyopo madarakani.

Kadhalika, Dkt. Migiro ametoa wito kwa viongozi wa ngazi zote za kitaifa kuhakikisha wanahudhuria vikao vya Chama katika ngazi za mashina, ili kujadili kwa pamoja utekelezaji wa ahadi walizozitoa kwa wananchi, kutatua changamoto zinazojitokeza na kulinda umoja wa Chama kama msingi wa kuendelea kusonga mbele na kuwatumikia wananchi.

Awali, akitoa shukrani kwa niaba ya wabunge waliohudhuria mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Mtumba na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema katika miaka ya hivi karibuni hakuna kipindi ambacho Chama kimewajali Mabalozi wa Mashina kama ilivyo katika Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM. Amewahimiza Mabalozi na viongozi wote wa Chama kuyatekeleza kwa vitendo maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM.






Post a Comment

0 Comments