URENO KUPELEKA WANAJESHI MSUMBIJI

Nchi ya Ureno itapeleka wanajeshi nchini Msumbiji katika kipindi cha nusu ya mwanzo ya mwezi Aprili kufuatia shambulizi la wanamgambo wa itikadi kali lililofanywa dhidi ya mji wa Palma. 

Wanajeshi hao wa Ureno watakuwa na jukumu la kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Msumbiji kwa mujibu wa ripoti iliyotangazwa na shirika la habari la Lusa ambalo limenukuu chanzo kutoka wizara ya ulinzi. 

Shirika hilo la habari la Ureno limesema makubaliano ya pande hizo mbili yanakamilishwa na kikosi maalum cha Ureno kitakuwa na wanajeshi 60 watakaopelekwa Msumbiji. 

Mapigano kati ya magaidi wa kundi linalojiita dola la kiislamu na wanajeshi wa Msumbiji yameingia siku ya saba baada ya wapiganaji hao wa itikadi kali kuutwaa mji wa pwani wa kimkakati kaskazini mwa nchi hiyo.

Mkurugenzi wa kampuni binafsi ya usalama,DAG,Max Dyck amesema mapigano yaliyoanza Jumatano wiki iliyopita bado yanaendelea. 

Taarifa zinaeleza kwamba maelfu ya wakaazi wa Palma bado wamekwama katika mji huo wakiwa wamejificha wakihangaika kutafuta njia kuondoka kwenye mji huo unaoshikiliwa na wapiganaji hao.

Post a Comment

0 Comments