ECOWAS KUJADILI MGOGORO MALI

Kanali Assimi Goita aliyetangazwa na Mahakama ya Katiba kuwa Rais wa Mali

***********

Viongozi na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), wanakutana Jumapili nchini Ghana kujadili mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Mali.

Rais Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane walijiuzulu baada ya kuwekwa kizuizini kwa siku kadhaa juma hili,katika mapinduzi ambayo yanatajwa kupangwa na Goita, ambaye alijitangaza kuwa rais mara moja,viongozi hao wa serikali ya mpito ya Mali Rais Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane waliachiwa baada ya kukaa kizuizini kwa muda wa siku tatu.

Na jamii ya kimataifa inaendelea kulishinikiza jeshi kurudisha utawala wa Serikali ya mpito inayoongozwa na raia kuelekea uchaguzi utakaozingatia Demokrasia baada ya mapinduzi ya mwaka jana.

ECOWAS imeonya juu ya kuweka tena vikwazo dhidi ya mwanachama mwenza Mali baada ya wanajeshi mapema wiki hii kuwashikilia viongozi wa serikali ya mpito iliyopewa jukumu la kuurudi utawala wa kiraia baada ya mapinduzi hayo ya Agosti mwaka uliopita.

Mahakama ya Katiba ya Mali ilimtangaza Kanali Assimi Goita,ambaye aliongoza mapinduzi ya kijeshi kuwa rais wa mpito,katika uamuzi wake mahakama hiyo imesema Goita anapaswa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Rais Bah Ndaw ambaye amejiuzulu.

Uamuzi huo unazidisha mkwamo ambapo viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi wanasema, unahatarisha harakati za kuelekea kwenye demokrasia na unadhoofisha mapambano dhidi ya makundi ya waasi.

ECOWAS yenye mataifa 15 imekuwa ikisimama na kutoa matamko imara katika mizozo kadhaa ya hivi karibuni katika eneo la Afrika Magharibi, iliweka vikwazo dhidi ya Mali baada ya maafisa vijana kumlazimisha kuachia madaraka rais aliyechaguliwa wa nchi hiyo, Ibrahim Boubacar Keita, baada ya kufanyika maandamano makubwa ya kumpinga.

Jumuiya hiyo iliisimamisha Mali kutoka kwenye vyombo vyake vya maamuzi, ilifunga mipaka yake na nchi hiyo na kusimamisha shughuli za fedha na biashara isipokuwa kwa bidhaa muhimu tu kama mafuta ya petroli na umeme.

Vikwazo hivyo viliondolewa baada ya serikali ya mpito kuundwa na kuwepo rais na waziri mkuu wa kiraia, na jeshi liliahidi kuurejesha utawala kamili wa raia ndani ya miezi 18.

Mali ni kati ya nchi masikini zaidi ulimwenguni huku ikiwa inapambana na waasi ambao walianza vurugu kwenye eneo la kaskazini mwa nchi hiyo mnamo mwaka 2012, baadaye uasi huo uliota mizizi na kuenea hadi katikati ya nchi hiyo na kisha kuvuka na kuingia katika nchi jirani za Niger na Burkina Faso,maelfu ya watu wamekufa na maelfu wengine wamekimbia makazi yao.

Post a Comment

0 Comments