POLISI WAPANDISHWA MAHAKAMANI KENYA

Maafisa sita  wa polisi nchini  Kenya jana Alhamisi wamefunguliwa mashitaka ya mauaji kutokana na vifo vya ndugu wawili wakati wakiwa kizuizini kwa tuhuma za kukiuka amri ya kutotoka nje kutokana na Covid. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP,mauaji ya Benson Njiru mwenye umri wa miaka 22 na nduguye Emmanuel Mutura Ndigwa mwenye umri wa miaka 19 yalipelekea maandamano makali,kulalamikia ukatili wa polisi.

Miongoni mwa maafisa 6 waliofunguliwa mashitaka,wawili kati ni wanawake na wote walikanusha mashitaka mahakamani huku wakiamuriwa wabaki rimande hadi Septemba 22 shauri la dhamana litakaposikilizwa.

Ndugu hao wanaodaiwa kuuwawa,walionekana mara ya mwisho Agosti mosi pale walipokamatwa na polisi kwa tuhuma za kuwa nje wakati wa curfew baada ya saa nne za usiku.

Miili yao ilipatikana siku mbili baadaye na wanafamilia kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha mji wa Embu kulingana na wanaharakati wa haki za binadamu.

Polisi wamedai kwamba wawili hao waliruka kutoka kwenye gari lao,madai ambayo yamekanushwa vikali na wanafamilia pamoja na wanaharakati.

Post a Comment

0 Comments