WARAIBU WAZINGATIWE WANAPOKABILIWA NA CHANGAMOTO

 


Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Godwin Mollel akimkabidhi tuzo mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa



Naibu Waziri wa Afya,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Godwin Mollel

********************

 Na Mashaka Mhando.

WARAIBU wawili kati ya 320 waliopo katika kituo cha matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya,kilichopo katika hospitali ya Bombo Jijini Tanga,wamefariki katika matukio tofauti baada ya kupatiwa matibabu.

Warahibu hao wamefariki kwa nyakati tofauti kwa kila mmoja na tukio lake, baada ya kufika katika kituo hicho ambacho tangu kijengwe na serikali mwaka jana kimekuwa msaada mkubwa kwa watu wanaotumia madawa ya kulevya.

Akitoa taarifa mwishoni mwa wiki katika tukio la kufunga kampeni ya kupambana na dawa za kulevya Jijini Tanga,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Jonathan Budemu alisema tangu kuanza kwa kituo hicho wamepata changamoto ya kuondokewa na wagonjwa wao wawili.

Alisema mmoja alifariki baada ya kuwa katika kituo akitumia dawa lakini alirudi mtaani na kuiba pikipiki alipokamatwa alishambuliwa na kupigwa hadi kupoteza maisha.

"Mgonjwa mmoja alirudi mtaani, aliiba pikipiki alikamatwa na wananchi walimshambulia kwa kipigo hadi akafa," alisema mganga mkuu.

Mwingine kwa maelezo ya Mganga Mkuu huyo ni kwamba baada ya kuwa anatumia dawa za kupunguza Uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya aina ya 'Methadone'alirudi mtaani akarudia kutumia madawa ya kulevya hadi akafariki.

"Huyu wa pili alifariki baada ya kupewa dawa ya Methadone akaenda kuongezea dawa za kulevya akaumwa alipofikishwa tena hapa kituoni alifariki," alisema Dkt Budemu.

Hata hivyo,alisema tangu serikali itoe kiasi cha shilingi milioni 763 kujengwa kituo hicho mwaka jana walianza kupokea vijana wawili karibu kila siku hadi sasa kufikia Warahibu 320 na wamekuwa wakitoa elimu katika wilaya za Tanga, Muheza na Korogwe kuelezea madhara ya kutumia madawa ya kulevya.

Aliitaka jamii ishiriki kikamilifu katika kutoa elimu kuhusu madhara yatokanayo na madawa ya kulevya kutokana na kuwa na athari kimwili kwa vijana lakini pia wanashiriki vitendo vya kihalifu kwa jamii kwa kuwadhuru.

"Sikuwahi kumuona mtu anayetumia madawa kabla sijahamishiwa hapa Tanga, lakini kiukweli nimewaona na imenisikitisha sana wanalala mapangoni kule baharini," alisema Budemu.

Katika kikao hicho ambacho mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Godwin Mollel mganga mkuu huyo aliiomba serikali mambo mawili kwanza kuwapatia miradi ya kufanya vijana wanaotumia dawa za kuacha kutumia madawa hayo pindi wanapopona lakini pia kujengwa kituo kingine kati ya Muheza au Korogwe ili kuwapunguzia mwendo mrefu kwenda Bombo kufuata matibabu.

"Waathirika hawa wanapopona wawezeshwe ili waweze kujikimu na maisha kwa kufanya kazi ndogo ndogo za biashara au ujasiriliamali," alisema Dkt Budemu.

Kuhusu kuweka kituo Korogwe au Muheza Dkt Budemu alisema kwa sasa wapo waathirika 16 kutoka maeneo hayo ambao kila mara wanafika katika kituo hicho kilichopo Bombo hivyo aliomba wajengewe ili kuwapunguzia gharama za nauli za kila mara za kufika Tanga.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Waziri, alitaka ndani ya wiki moja kifunguliwe kituo katika maeneo hayo ili kiweze kutoa huduma za dawa hizo za kupunguza uraibu kwa vijana.

Lakini pia Naibu Waziri aliwapongeza waandaji wa kampeni hiyo kwa kuweza kusaidia kupungua kwa watumiaji wa dawa za kulevya lakini pia kuweka mkakati mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii.

Post a Comment

0 Comments