VIONGOZI kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mkoani Geita wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Peter Bura, Katibu Tawala wa Wilaya pamoja na madiwani wa halmashauri hiyo wamefanya ziara ya mafunzo Shamba la Miti Saohill lililopo Wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa.
Akizungumsha wakati wa ukaribisho wa Viongozi hao Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt Linda Salekwa amewapongeza kwa kuchagua kuja kutembelea na kujifunza kuhusu uhifadhi wa misitu utunzaji mazingira na ukusanyaji wa mapato katika Wilaya ya Mufindi kwani ni eneo sahihi kwao.
“Tunapozungumza habari ya uhifadhi wa misitu, na ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na serikali kwa ujumla, Wilaya ya Mufindi imepiga hatua kubwa sana na hii inatokana na uwepo wa Shamba la Miti la serikali la Saohill” Amesema Dkt. Linda Salekwa
Ameongeza kuwa kupitia elimu inayotolewa na wahifadhi kuhusu utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti imechangia uwepo wa rasilimali kubwa ya misitu hali iliyopelekea kuwepo kwa viwanda vingi vinavyochakata mazao ya misitu na hivyo kuongeza pato la mwananchi mmojammoja na taifa na hii ni kutokana na uuzaji na ushuru unaokusanywa kupitia mazao ya misitu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Peter Bura amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza ni kwa namna gani Wilaya ya Mufindi kupitia Shamba la Miti Saohill wamefanikiwa katika uhifadhi wa misitu na ukusanyaji wa mapato ili nao waweze kuona ni hatua gani watazichukua katika kufanikisha hilo katika Wilaya ya Chato.
“Katika Wilaya ya Chato tunalo Shamba la Miti Silayo hivyo tumekuja kujifunza ni kwa namna gani wenzetu wa Mufindi wananufaika vipi kimazingira na kimapato ili na sisi kupitia Shamba la Miti Silayo tuone namna tutakavyoshirikiana na TFS katika kuleta tija wilayani kwetu kupitia Shamba lile” Amesema Mkuu wa Wilaya ya Chato
Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Saohill PCO Tebby Yoramu amesema kuwa Shamba limefanikiwa kufika hatua iliyopo kwa sasa kutokana na kuwepo kwa programu mbalimbali zinazolenga kujenga mahusiano mazuri na jamii zinazolizunguka shamba ikiwemo kutoa ajira za kutwa kwa wananchi, elimu ya uhifadhi pamoja na kusaidia shughuli za maendeleo katika sekta ya elimu, afya na miondombinu ya barabara hali inayopelekea kuwepo kwa uhusiano chanya baina ya shamba, taasisi na wananchi.
Katika ziara hiyo Viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chato waliweza kujifunza juu ya shughuli mbalimbali za ufugaji nyuki, uzalishaji wa miche katika bustani, pamoja na shughuli za uvunaji wa utomvu katika misitu ya kupandwa.
0 Comments