Rais Mstaafu Kikwete Aungana na Waumini Kumuaga Kardinali Pengo

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, leo ameungana na waumini wa Kanisa Katoliki na wananchi wengine kuomboleza kifo cha Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwa kuweka saini katika kitabu cha maombolezo kilichofunguliwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.

Baada ya zoezi hilo, Dkt. Kikwete alimpa pole Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Thaddaeus S. Ruwa’ichi, pamoja na viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki, akisema marehemu ameacha alama kubwa katika historia ya Kanisa na Taifa la Tanzania.

Akizungumza na vyombo vya habari, Kikwete alisema alimfahamu Kardinali Pengo kwa muda mrefu tangu miaka ya awali ya utumishi wake serikalini, akimtaja kama kiongozi mwenye busara, imani thabiti na moyo wa kujitoa kwa jamii.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Kardinali Pengo alifariki dunia Februari 19, 2026 akiwa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.

Ratiba ya mazishi inaonyesha kuwa waombolezaji wataendelea kutoa heshima za mwisho katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu kabla ya mwili kuhamishiwa Kituo cha Hija Pugu, ambako Misa ya Mazishi itafanyika kuhitimisha shughuli zote za mazishi.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5, 1944, akapadrishwa mwaka 1971 na baadaye kutangazwa kuwa Kardinali mwaka 1998 na Papa Yohane Paulo II. 

Alistaafu rasmi mwaka 2019 baada ya miaka mingi ya utumishi wa kiroho na uongozi ndani ya Kanisa Katoliki.

Post a Comment

0 Comments