Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeingia makubaliano ya ushirikiano na kampuni ya uchimbaji madini ya Afrika Kusini ya Plantcor Mining and Plant Hire kwa lengo la kuendeleza uchimbaji wa dhahabu katika leseni zake za Kigosi, zilizopo wilayani Bukombe,mkoani Geita.
Hafla ya utiaji saini ilifanyika Februari 23 na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa, pamoja na viongozi wa Mkoa wa Geita na Wilaya ya Bukombe, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kukuza sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Venance Mwasse, alisema ubia huo unalenga kuongeza uzalishaji wa dhahabu kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ikiwemo kufanya tafiti za anga (airborne survey) ili kubaini kwa usahihi taarifa za kijiolojia za eneo la Kigosi.
Aliongeza kuwa mradi huo utafungua ajira kwa wananchi wa Bukombe na maeneo jirani, huku akisisitiza utekelezaji wa sera ya Local Content ili kuhakikisha wazawa wananufaika moja kwa moja na rasilimali za eneo lao.
Kwa upande wake, Dkt. Kiruswa aliitaka STAMICO kuhakikisha mradi unazingatia viwango vya utunzaji wa mazingira, uwajibikaji kwa jamii (CSR) na usimamizi wa uwazi, akisisitiza kuwa maendeleo ya mradi yanapaswa kwenda sambamba na ustawi wa jamii inayouzunguka.
Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Simon Sirro, alisema makubaliano hayo yanaimarisha mazingira ya uwekezaji nchini na yanafanyika kwa kuzingatia sheria na maslahi ya Taifa.
Naye Mtendaji Mkuu wa Plantcor, Josef Wilmans, alisema kampuni hiyo italeta utaalamu wa kiufundi na kifedha ili kuongeza tija na kuimarisha uzalishaji wa dhahabu, sambamba na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, aliahidi ushirikiano wa karibu wa Serikali ya Mkoa katika kuhakikisha mradi unafanikiwa, huku Mbunge wa Bukombe, Dotto Mashaka Biteko, akiwataka wananchi kujipanga kuchangamkia fursa zitakazozalishwa na mradi huo kwa maendeleo ya wilaya na Taifa kwa ujumla.


0 Comments