Rais wa Marekani, Donald Trump, ameagiza jeshi la nchi hiyo kuharibu boti ndogo za Iran zinazopita katika eneo la Mlango wa Bahari wa Strait of Hormuz, akisisitiza kulinda usalama wa njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.
Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump amesema pia kuwa jeshi la Marekani linaongeza operesheni za kuondoa mabomu yaliyotegwa katika njia hiyo, ili kuhakikisha usafirishaji wa mafuta unaendelea bila vikwazo.
Kauli hiyo inakuja wakati Jeshi la Marekani likidai kukamata meli nyingine ya mafuta inayodaiwa kusafirisha mafuta ya Iran kwa njia ya magendo katika Bahari ya Hindi, hatua inayozidi kuongeza mvutano kati ya pande hizo mbili.
Wakati huo huo, Iran imeonekana kuongeza udhibiti wake katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, baada ya kusambaa kwa video zinazoonesha wanajeshi wake wakikagua na kuisimamia meli kubwa ya mizigo katika eneo hilo.
Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa mvutano katika ukanda wa Mashariki ya Kati, huku kila upande ukionekana kuchukua hatua za kuimarisha ushawishi na ulinzi katika njia hiyo nyeti ya kimataifa.

0 Comments