Takriban watu 21 wamepoteza maisha kufuatia ajali ya moto iliyotokea katika hoteli moja jijini New Delhi nchini India, huku zaidi ya watu 40 wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Kwa mujibu wa polisi wa Delhi, moto huo ulizuka katika Hoteli ya Flourish Stay iliyopo kusini mwa mji huo. Miongoni mwa waliofariki wanadaiwa kuwemo baadhi ya raia wa Afrika waliokuwa wamefika nchini India kwa ajili ya matibabu.
Polisi wameeleza kuwa ajali hiyo ni miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya moto kuwahi kutokea katika mji mkuu huo katika miaka ya hivi karibuni.
Zoezi la uokoaji na utafutaji wa manusura bado linaendelea, huku vikosi vya zimamoto vikifanikiwa kuudhibiti moto huo kwa kutumia magari manane ya kuzimia moto.
Chanzo cha moto huo bado hakijabainika, ingawa hitilafu za umeme zimekuwa zikitajwa mara kwa mara kuwa chanzo kikuu cha ajali za moto nchini India.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliofariki na kueleza masikitiko yake kufuatia tukio hilo.
Ajali za moto zimekuwa zikitokea mara kwa mara nchini India kutokana na changamoto za usalama wa majengo na ukosefu wa vifaa vya kutosha vya kuzimia moto.

0 Comments