Masoko ya Madini Katoro na Geita Yachochea Uchumi, Yafungua Fursa za Ajira

 

Masoko ya Madini ya Katoro na Geita pamoja na vituo vya ununuzi wa madini yanaendelea kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Geita kwa kuongeza fursa za ajira, kuimarisha biashara na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha katika jamii zinazozunguka maeneo ya shughuli za madini.

Akizungumza kuhusu mchango wa masoko hayo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Mjiolojia Samwel Shoo, amesema kuwa uwepo wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini umeimarisha biashara halali kwa kuweka mfumo wa bei elekezi unaolinda maslahi ya wachimbaji wadogo na kuongeza uwazi katika biashara ya madini.

Ameeleza kuwa kupitia mfumo huo, wachimbaji wadogo wameweza kuuza madini yao kwa bei yenye ushindani, hali iliyoongeza kipato chao na kuwasaidia kuboresha maisha yao, ikiwemo kugharamia elimu, afya na makazi bora.

Mjiolojia Shoo ameongeza kuwa kuongezeka kwa shughuli za masoko ya madini kumevutia wafanyabiashara, wasafirishaji na watoa huduma mbalimbali, hatua iliyochochea ukuaji wa biashara ndogondogo, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake, pamoja na kuimarisha uchumi wa maeneo hayo.

Kwa ujumla, amesema kuwa masoko hayo yamechangia kuongeza mapato ya Serikali, kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kuhimiza maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Geita.

Post a Comment

0 Comments