Tanzania na Urusi Kuongeza Ushirikiano wa Biashara na Uwekezaji


Na Beda Msimbe, TBN, Moscow

Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin, amesema nchi yake itaendelea kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi na uwekezaji kwa Tanzania kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Putin amesema kwa sasa Urusi ina miradi zaidi ya 70 nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 434.22, ambayo imechangia kutoa ajira zaidi ya 3,000 kwa Watanzania. Ameongeza kuwa fursa zaidi zitatangazwa katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaotarajiwa kufanyika nchini Urusi katika siku zijazo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Putin amesema Urusi imekuwa ikifuatilia kwa karibu mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayotekelezwa nchini Tanzania na kuridhishwa na hatua ya maendeleo inayofikiwa.

Amesema mazungumzo yao yamekuwa na tija kubwa na yamejikita katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara, uwekezaji na maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema ziara yake nchini Urusi ina umuhimu mkubwa wa kihistoria kwa Tanzania, ikizingatiwa kuwa ni zaidi ya miaka 50 imepita tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiongozi wa Tanzania nchini humo.

Rais Samia ameeleza kuwa ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi katika sekta mbalimbali za maendeleo, huku akitoa shukrani kwa Rais Putin na Serikali ya Urusi kwa mwaliko na mapokezi mazuri.

Aidha, Rais Samia amekumbusha mchango wa Urusi katika harakati za Tanzania za kupigania uhuru na kumpongeza Rais Putin kwa maadhimisho ya miaka 81 ya Ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia yaliyofanyika Mei mwaka huu.

Viongozi hao wameeleza dhamira yao ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano wa pande mbili, pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa mataifa yao.

Post a Comment

0 Comments