Sierra Leone Kupokea Wahamiaji 25 Waliorejeshwa Kutoka Marekani

Sierra Leone inatarajiwa kupokea kundi la kwanza la wahamiaji wanaorejeshwa kutoka Marekani siku ya Jumatano, ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump wa kuwarejesha wahamiaji katika mataifa yanayoendelea.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone, Timothy Musa Kabba amesema ndege ya kwanza yenye wahamiaji 25 itawasili katika mji mkuu wa Freetown Jumatano asubuhi. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya makubaliano ya nchi hiyo kupokea hadi wahamiaji 300 kwa mwaka kutoka ukanda wa Afrika Magharibi.

Sierra Leone ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyofikia makubaliano kama hayo na Marekani, pamoja na Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Eswatini, Equatorial Guinea, Ghana, Rwanda na Sudan Kusini.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Kabba amesema baadhi ya wahamiaji hao wana asili ya Afrika Magharibi na wengine waliwahi kuwa na nyaraka za Sierra Leone miaka iliyopita.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, wahamiaji wataruhusiwa kukaa Sierra Leone kwa muda wa siku 90 kabla ya kurejea katika nchi zao za asili.

Serikali ya Marekani pia inatarajiwa kutoa msaada wa dola milioni 1.5 kugharamia huduma za kibinadamu na uendeshaji wa mpango huo. Mara nyingi mataifa yanayokubali kupokea wahamiaji kutoka Marekani hupatiwa msaada wa kifedha kama sehemu ya makubaliano hayo.

Post a Comment

0 Comments