Mgomo wa wahudumu wa usafiri wa umma nchini Kenya umesitishwa kwa muda wa wiki moja ili kutoa nafasi kwa mazungumzo kati ya serikali na wadau wa sekta hiyo, baada ya maandamano ya siku mbili kusababisha vifo vya watu wanne na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa.
Maamuzi hayo yalitangazwa Jumanne baada ya mazungumzo ya awali kuvunjika Jumatatu, ambapo wahudumu wa usafiri walitaka serikali kupunguza bei ya mafuta ili kupunguza gharama za uendeshaji na nauli kwa abiria.
Katika siku mbili za mgomo huo, abiria wengi walikwama baada ya magari ya usafiri wa umma kusimamisha huduma huku baadhi ya waandamanaji wakiziba barabara na kuchoma matairi wakipinga ongezeko la bei ya mafuta.
Serikali ya Kenya imeeleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kumesababishwa na athari za vita vya Iran vilivyoathiri upatikanaji wa nishati duniani. Bei ya dizeli iliongezeka kwa asilimia 23.5 kuanzia Ijumaa iliyopita.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen amesema serikali itafanya mazungumzo na wadau wa sekta ya mafuta ndani ya siku saba zijazo ili kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu bei ya mafuta.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wahudumu wa usafiri, Kennedy Kaunda amesema wamekubali kusitisha mgomo huo kwa muda ili kutoa nafasi kwa mazungumzo, lakini iwapo hakutakuwa na muafaka watarejea kutoa maelekezo mengine kwa umma baada ya wiki moja.
Aidha, watu 348 wamekamatwa kuhusiana na mgomo huo na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kushiriki mgomo usio halali.

0 Comments