UN Yataja Mauaji ya Kimbari Al Fasher,Yawaadhibu Viongozi wa RSF

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza vikwazo dhidi ya makamanda wanne wa Rapid Support Forces (RSF) kwa tuhuma za ukatili walioufanya wakati wa kuuteka mji wa Al Fasher katika jimbo la Darfur, nchini Sudan, mwezi Oktoba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliowekewa vikwazo ni naibu makamanda wa RSF Abdelrahim Hamdan Daglo na Gedo Hamdan Ahmed, pamoja na Brigedia Jenerali Al-Fateh Abdullah Idris na kamanda wa uwanja Tijani Ibrahim.

Hatua hiyo inafuatia ripoti ya uchunguzi wa UN iliyobaini kuwa RSF ilihusika katika vitendo vilivyotajwa kuwa ni mauaji ya kimbari wakati wa kuzingira kwa miezi 18 mji wa Al Fasher kabla ya kuuvamia rasmi Oktoba 26. Tangu Aprili 2023, Sudan imekumbwa na vita kati ya RSF na jeshi la kawaida la nchi hiyo, hali ambayo UN imeitaja kuwa ni “vita vya ukatili,” vilivyosababisha maelfu ya vifo na janga kubwa la njaa na wakimbizi.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, RSF iliuzingira mji wa Al Fasher, ambao ulikuwa ngome ya mwisho ya Darfur Kaskazini iliyokuwa nje ya udhibiti wao. Ujumbe wa uchunguzi wa UN uliita operesheni ya kuuteka mji huo kuwa ni “siku tatu za hofu,” zikihusisha mauaji ya papo kwa papo, ukatili wa kijinsia uliopangwa na utekaji wa raia, hasa wa kabila la Zaghawa.

Taarifa ya vikwazo inaeleza kuwa Abdelrahim Hamdan Daglo, ambaye ni ndugu wa kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Daglo, alionekana katika video akitoa maagizo kwa wapiganaji wake kutowachukua mateka bali kuwaua. Tayari amekwishawekewa vikwazo na Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Kwa upande wake, Al-Fateh Abdullah Idris, maarufu kwa jina la Abu Lulu, alipewa jina la “Mwauaji wa Al-Fasher” kutokana na video alizojirekodi akifanya mashambulizi. Baraza la Usalama lilisema alionekana akicheka huku akitekeleza mauaji, yakiwemo yale yaliyolenga watu kwa misingi ya kikabila.

Wiki iliyopita, Marekani pia iliwawekea vikwazo Idris, Ahmed na Ibrahim kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya kikabila, mateso, njaa na ukatili wa kijinsia. Maamuzi ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa hufanywa na kamati maalum ya Baraza la Usalama yenye wawakilishi wa nchi zote 15 wanachama.

Post a Comment

0 Comments