Zambia:Mambwe Zimba Ashikiliwa Lusaka kwa Tuhuma za Uchochezi Mtandaoni

Katibu Mkuu wa chama cha National Democratic Congress (NDC), Mambwe Zimba, ameripotiwa kukamatwa na vyombo vya dola mjini Lusaka kwa tuhuma za kuhusika na usambazaji wa picha iliyotengenezwa kwa njia ya kidijitali ikimuonesha Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, akiwa katika jeneza.

Kwa mujibu wa ripoti ya Lusaka Times, picha hiyo inayodaiwa kuhaririwa ilimuonesha pia Makamu wa Rais, Mutale Nalumango, akitoa heshima za mwisho. Maudhui hayo yalichapishwa kwenye ukurasa wa Facebook unaojulikana kama “Zambia kwa Wote 2026.”

Taarifa zinaeleza kuwa Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni kilianza kufuatilia tukio hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa makosa hayo yanadaiwa kufanyika Lusaka, ingawa muda kamili haujawekwa wazi.

Polisi pia wanaripotiwa kukamata simu aina ya Samsung A24 inayohusishwa na uchunguzi huo. Kwa mujibu wa mamlaka, picha hiyo ilikusudia kupotosha umma na kusababisha taharuki katika jamii.

Kwa sasa, Zimba anazuiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Lusaka huku uchunguzi ukiendelea, na vyombo vya dola vimeeleza kuwa hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa kadri uchunguzi utakavyokamilika.

Post a Comment

0 Comments