FCC na BoT Kushirikiana Kulinda Walaji wa Huduma za Kifedha

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, amesema kuwa katika kipindi cha robo mwaka Tume hiyo imepokea jumla ya malalamiko 63 kutoka kwa wananchi, ambapo malalamiko 45 tayari yamepatiwa ufumbuzi huku malalamiko 19 yakiwa bado katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa.

Akizungumza Machi 5, 2026 katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma, Ngasongwa amesema kuwa Tume hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda maslahi ya walaji pamoja na kuhakikisha ushindani wa haki katika masoko mbalimbali nchini.

Ameeleza kuwa mbali na kupokea na kushughulikia malalamiko ya watumiaji, Tume ya Ushindani pia ina jukumu la kusajili na kupitia mikataba mbalimbali kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha inazingatia taratibu zilizowekwa na inalinda maslahi ya walaji pamoja na sekta ya kifedha.

Ngasongwa amesisitiza kuwa taasisi za fedha, hasa zinazotoa huduma za mikopo, haziruhusiwi kuongeza viwango vya riba au kufanya mabadiliko katika mifumo yao bila kupata kibali kutoka Tume ya Ushindani kwa kuzingatia taratibu zilizopo.

Aidha, amesema Tume hiyo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili njia bora za kuwalinda walaji, hususan katika sekta ya huduma za kifedha ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi.

Amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha huduma jumuishi za kifedha pamoja na kuweka mifumo madhubuti ya kushughulikia malalamiko ya wateja ili kuhakikisha wanapata huduma bora na zenye haki.

Katika hatua nyingine, Ngasongwa amesema Tume imefanya kazi kwa kushirikiana na Wakala wa Vipimo pamoja na wadau wengine kufuatilia malalamiko ya watumiaji wa huduma za intaneti, ambapo wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia matumizi ya vifurushi vya data.

Ameongeza kuwa tafiti zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha wananchi wanapata thamani halisi ya fedha wanazolipia kulingana na kiwango na ubora wa huduma wanazopokea.

Kwa mujibu wa Ngasongwa, hatua hizo pia zinalenga kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuhakikisha ushindani huru na wa haki unaendelea kuimarika pamoja na kukuza uchumi wa soko.

Aidha, amesema katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, Tume inalenga kuimarisha ushindani wa kibiashara ili kuongeza uwezo wa ununuzi kwa wananchi na kuchochea mzunguko wa fedha katika uchumi.

Ngasongwa pia ameeleza kuwa Tume imeandaa programu ya maadhimisho ya Haki za Mlaji, ambapo kilele chake kitafanyika Machi 31 mwaka huu. Maadhimisho hayo yatahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo kliniki za watumiaji pamoja na mikutano itakayojadili masuala ya chakula na lishe.

Amesema maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha matumizi salama ya bidhaa na huduma ili kuhakikisha walaji wanapata usalama wa vyakula na huduma wanazotumia.

Pia amebainisha kuwa Tume itaandaa vikao vya uelimishaji vitakavyowahusisha wazalishaji, walaji pamoja na Serikali kwa lengo la kujadili masuala muhimu yatakayosaidia kuboresha sekta mbalimbali za kiuchumi.

Kwa upande mwingine, amesema Tume inaendelea kutekeleza miradi ya kidijitali kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kupitia mfumo wa Automation of Business Process.

Ameongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, Tume imeingia ubia na taasisi ya TradeMark Africa ambapo kiasi cha dola za Marekani 600,000, sawa na takribani shilingi bilioni 1.4, kimetengwa kwa ajili ya kuboresha mifumo ya utoaji huduma pamoja na kuimarisha udhibiti wa bidhaa bandia nchini.

Post a Comment

0 Comments