TEMESA Yaonesha Mafanikio yake Katika Maonesho ya Siku 100 Jijini Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ametembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika maonesho ya mafanikio ya siku 100 za uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yakiangazia utatuzi wa kero za wananchi.

Maonesho hayo ya siku tatu yamefunguliwa Machi 5 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma na yamehudhuriwa na taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo TEMESA, ambayo imeonesha mafanikio yake katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kutoa elimu kuhusu majukumu yake.

Akiwa katika banda la TEMESA, Mhe. Senyamule alipokea maelezo kuhusu shughuli za Wakala huo pamoja na mafanikio yake kutoka kwa Meneja Masoko na Uhusiano wa Umma, Bi. Martha Joachim.

Bi. Martha amesema TEMESA imepiga hatua katika kuboresha huduma za kiufundi kwa taasisi za Serikali kupitia matumizi ya mifumo ya kisasa na kidijitali, ikiwemo Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM) unaorahisisha ufuatiliaji wa shughuli za matengenezo kwa ufanisi.

“Mfumo huu umeongeza uwazi, ufanisi na kasi katika utoaji wa huduma za matengenezo, na kusaidia taasisi za Serikali kupata huduma bora zinazowawezesha kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi,” amesema Bi. Martha.

Aidha, ameongeza kuwa TEMESA inaendelea kuboresha huduma zake, hususan katika matengenezo ya magari ya Serikali, usimamizi wa vivuko, pamoja na miundombinu ya umeme katika taasisi mbalimbali za umma.

Post a Comment

0 Comments