OWM-Kazi Yapata Baraka za Kamati ya Bunge kwa Bajeti ya 2026/27


Na. OWM-KAM,Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeridhia mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku ikipongeza utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/2026.

Akizungumza baada ya majadiliano ya kamati hiyo Bungeni jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Hawa Mchafu, amesema wameridhishwa na namna wizara hiyo ilivyowasilisha na kutekeleza majukumu yake.

Amesema miongoni mwa maeneo yaliyopongezwa ni usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kiwanda cha chai Mponde, kiwanda cha ngozi cha Kilimanjaro (KLICL), mradi wa jengo la kitega uchumi Mzizima pamoja na mafunzo ya uanagenzi katika Chuo cha Wananchi Kigamboni na mfumo wa kielektroniki wa e-UTATUZI.

Pamoja na pongezi hizo, kamati imeitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuongeza nafasi za vijana wanaopata mafunzo ya ujuzi kupitia programu za uanagenzi, pamoja na kusimamia kwa karibu fursa za ajira nje ya nchi ili kuhakikisha Watanzania wanapata mikataba yenye tija na malipo stahiki.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameomba kamati hiyo kupitisha bajeti ili kuiwezesha serikali kuendelea kutekeleza mipango ya kukuza ajira, kutoa huduma kwa wananchi na kusimamia miradi ya maendeleo.

Amesema utekelezaji wa shughuli hizo utaendana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aidha, Waziri Sangu ameeleza kuwa serikali itaendelea kuzingatia sheria, taratibu na miongozo katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuhakikisha wananchi wananufaika na matunda ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kadhalika, amebainisha kuwa serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa e-UTATUZI kwa ajili ya kusajili na kutatua migogoro ya kikazi, huku akiongeza kuwa wabunge watapatiwa mafunzo maalum ili wawe mabalozi wa kuhamasisha wananchi kutumia mfumo huo kufikisha malalamiko yao bila kulazimika kusafiri kwenda ofisi za Tume ya Usuluhishi na Utatuzi (CMA).

Post a Comment

0 Comments