RC Batilda ashiriki Swala ya Eid El Fitri,Asisitiza Ulinzi wa Watoto Wakati wa Sherehe


Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt.Batilda Burian amewataka wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao wanapokwenda kutembea wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Eid El Fitri, ili kuepuka ajali na matukio yasiyotarajiwa.

Akizungumza jana baada ya kumalizika kwa Swala ya Eid El Fitri katika Msikiti wa Ijumaa jijini Tanga, Dkt. Batilda alisema ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha watoto wanakuwa chini ya uangalizi wa karibu wanapokuwa nje kusherehekea sikukuu hiyo.

Alisisitiza kuwa uangalizi huo utasaidia kuhakikisha watoto wanatembea kwa usalama na kusherehekea sikukuu kwa amani, bila kukumbwa na madhara yanayoweza kusababisha huzuni au hata vifo.

“Wazazi na walezi niwaombe, wakati wa sikukuu watoto wanapokwenda kutembelea, wawe chini ya uangalizi wa watu wazima. Hata njiani tuwe makini kwa sababu kuna vyombo vya usafiri kama bodaboda na magari. Tuhakikishe tunasherehekea sikukuu kwa usalama bila kadhia itakayoweza kuleta majonzi na misiba,” alisema Dkt. Batilda.

Aidha,aliwataka wakazi wa Mkoa wa Tanga kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kijamii, pamoja na kuendeleza upendo miongoni mwao.

Pia aliwahimiza wananchi kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine wa dini na serikali.

Katika kuhitimisha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wananchi kuendeleza mila nzuri za sikukuu hiyo ikiwemo kuwatembelea wagonjwa, ndugu na jamaa, pamoja na kuzuru makaburi na kufanya matendo ya huruma.

“Nitoe salamu za Eid El Fitri kwa wana Tanga na Watanzania kwa ujumla. Tuendelee kufanya yale tuliyofundishwa, kuwatembelea wagonjwa, ndugu na jamaa, kuzuru makaburi, kufanya amali njema na kudumisha upendo miongoni mwetu,” alisisitiza.


Post a Comment

0 Comments