Eid El Fitri:Makubel Awasihi Wana Tanga Kulinda Mali Zao Kwenye Wimbi la Maendeleo

Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Kassim Amary Makubel, amewatakia heri ya Sikukuu ya Eid El Fitri wakazi wa jiji hilo, huku akibainisha kuwa Tanga imeanza kufunguka kimaendeleo na itaendelea kupiga hatua zaidi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.

Akizungumza katika salamu zake za sikukuu, Makubel alisema kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa imeanza kuleta matokeo chanya, hali inayofanya jiji hilo kuvutia wawekezaji na kukuza uchumi wa wananchi.

Alisema ni muhimu kwa wakazi wa Tanga kuitumia fursa hiyo kwa manufaa yao binafsi na ya vizazi vijavyo kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo zinazoibuka.

Aidha, aliwashauri wananchi kutojiharakisha kuuza nyumba zao, hususan zile za urithi, kwa kuwa zinaweza kuwa na thamani kubwa zaidi siku zijazo kadri maendeleo yanavyozidi kushika kasi.

Makubel alieleza kuwa badala ya kuuza mali hizo, wananchi wanaweza kuingia ubia na wawekezaji kwa kipindi maalum, jambo litakalowawezesha kunufaika na thamani ya maeneo yao bila kupoteza umiliki.

Alionya kuwa kuuza mali kiholela kunaweza kusababisha baadhi ya wananchi kujikuta wakihama kutoka maeneo ya katikati ya jiji na kuishi nje ya mji, hali itakayopunguza fursa zao za kiuchumi.

Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na uelewa mpana kabla ya kufanya maamuzi ya kuuza mali zao, ili kuepuka hasara zisizo za lazima.

Katika kuhitimisha, Mbunge huyo aliwataka wakazi wa Tanga kuendelea kudumisha amani, mshikamano na kutumia kipindi cha sikukuu kufanya matendo mema pamoja na kusaidiana.

Post a Comment

0 Comments