Mwanza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amewataka watendaji wa Tume ya Madini hususan Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuimarisha usimamizi wa mazingira katika shughuli za uchimbaji madini kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara, hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua, ili kuzuia ajali zinazoweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo.
Mhandisi Samamba ametoa wito huo wakati akifungua Kikao cha Pili cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Tume ya Madini kilichofanyika jijini Mwanza, kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, viongozi kutoka Wizara ya Madini, Ofisi ya Kamishna wa Kazi, TUGHE pamoja na wakurugenzi, mameneja na wawakilishi wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Amesisitiza kuwa usalama wa wachimbaji unapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwa watendaji wote wa sekta ya madini, akieleza kuwa uhai wa mchimbaji mmoja una thamani kubwa kwa Taifa.
“Ni wajibu wenu kuhakikisha maeneo yote ya uchimbaji yanakaguliwa mara kwa mara na migodi yenye vihatarishi vya ajali inafungwa mara moja, lengo likiwa ni kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali za madini bila kuhatarisha maisha yao,” amesema Mhandisi Samamba.
Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini kuanzia uchimbaji, uchenjuaji hadi biashara ya madini, hatua itakayosaidia kuongeza uwazi, kudhibiti mianya ya rushwa na kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki. Ni
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili na uadilifu kazini ili kuendelea kujenga taswira chanya ya Tume ya Madini mbele ya wananchi na wadau wa sekta hiyo.
Akizungumzia mafanikio ya ukusanyaji wa maduhuli, Mhandisi Samamba ameipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka malengo ya makusanyo ambapo kuanzia Julai 2025 hadi Machi 24, 2026 imekusanya zaidi ya shilingi trilioni moja, sawa na zaidi ya asilimia 111 ya lengo la kipindi husika.
Ameeleza kuwa kasi hiyo inaipa Tume matumaini ya kuvuka lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.2 ifikapo Juni mwaka huu katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026, fedha zitakazochochea maendeleo ya huduma za jamii ikiwemo umeme, maji, barabara, shule na sekta nyingine muhimu kwa wananchi.
Ameongeza kuwa kumekuwepo na ongezeko la uzalishaji wa madini ya dhahabu kutoka tani 54.06 zenye thamani ya shilingi trilioni 7.004 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 hadi tani 66.88 zenye thamani ya shilingi trilioni 12.265 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 na kusisitiza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2025 hadi Februari 2026 jumla ya tani 46.24 zenye thamani ya shilingi trilioni 11.726 zilizalishwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amesema mafanikio ya Tume yanaonekana wazi kupitia ongezeko la makusanyo ya maduhuli kutoka shilingi bilioni 360 mwaka wa fedha 2017/2018 hadi kufikia shilingi trilioni 1.072 mwaka 2024/2025, hali inayoonesha mchango mkubwa wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, ameishukuru Wizara ya Madini kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi kupitia uboreshaji wa maslahi pamoja na kuongeza vitendea kazi ikiwemo magari na kompyuta zilizogawiwa katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwakilishi wa Kamishna wa Kazi, Betty Mtega pamoja na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Mkoa wa Dodoma, Samwel Nyungwa, wameipongeza Tume ya Madini kwa kuimarisha utaratibu wa vikao vya Baraza la Wafanyakazi vinavyotoa fursa kwa watumishi kushiriki kikamilifu kutoa maoni ya maboresho ya rasimu ya bajeti kabla ya kuwasilishwa rasmi.




0 Comments