TMA Yatoa Tahadhari ya Mafuriko na Upungufu wa Unyevu Nchini

 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya uwezekano wa kutokea kwa mafuriko na vipindi vya upungufu wa unyevu katika mikoa mbalimbali nchini, kufuatia mwelekeo wa mvua za masika zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Februari hadi Mei.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 5, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa mikoa ya Kagera na Geita, inayojumuisha ukanda wa magharibi mwa Ziwa Victoria, inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu kidogo ya wastani.

Mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyanga inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini kidogo ya wastani.

Aidha, amesema kuwa mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, inayojumuisha nyanda za juu kaskazini mashariki, inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini kidogo ya wastani, huku mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani pamoja na visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba ikitarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu kidogo ya wastani kuanzia katikati ya Machi hadi mwishoni mwa Mei.

Dkt. Chang’a amebainisha kuwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kuna uwezekano wa kutokea mvua kubwa za ghafla katika maeneo yote, ikiwemo yale yanayotarajiwa kupata mvua chache. Tathmini inaonesha kuwa mvua zinaweza kuongezeka kuelekea mwezi Aprili, hali inayoweza kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo.

Kwa upande wa sekta ya kilimo, amesema mikoa inayotarajiwa kupata mvua nyingi, ikiwemo Kagera na Geita, inaweza kukumbwa na mafuriko na kuathiri uzalishaji wa mazao. Vilevile, mikoa yenye mvua chache kama Mara na Mwanza inaweza kukabiliwa na upungufu wa unyevu na kusababisha mavuno duni.

Sekta ya afya inatarajiwa kukabiliwa na hatari ya kuongezeka kwa magonjwa yatokanayo na maji kutuama, hususan katika mikoa ya pwani na nyanda za juu kaskazini mashariki. Aidha, baadhi ya maeneo yanaweza kukumbwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Sekta ya usafiri nayo inaweza kuathiriwa, hasa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Pwani, ambako mvua nyingi zinaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na kuchelewesha huduma za usafiri.

Kwa ujumla, Dkt. Chang’a amesisitiza umuhimu wa wananchi na taasisi za serikali kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuchukua tahadhari zinazotolewa na TMA ili kupunguza athari za mafuriko, upungufu wa unyevu na milipuko ya magonjwa inayoweza kujitokeza katika msimu huu wa mvua za masika.

Post a Comment

0 Comments