Rais Samia Afungua Milango ya Fursa Dubai


Dubai,UAE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumanne, Februari 3, 2026, ameanza ziara ya kikazi jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa kufanya mazungumzo na viongozi na wadau wa kimataifa, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja nchini.

Katika ratiba ya siku ya kwanza ya ziara hiyo, Rais Samia anakutana na Waziri Mkuu wa Antigua and Barbuda, Mhe. Gaston Browne, pamoja na kufanya mazungumzo ya pande mbili na Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism), Bi. Shaikha Al Nuwais.

Mazungumzo hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kukuza sekta ya utalii, biashara na uwekezaji, pamoja na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa Tanzania.

Aidha, jioni ya leo Rais Samia anatarajiwa kushiriki katika uzinduzi wa Global Africa Investment Summit (GAIS), jukwaa la uwekezaji linalolenga kuoanisha miradi iliyo tayari kuwekezeka barani Afrika na wawekezaji wa kimataifa.

Mkutano huo unaendeshwa sambamba na majadiliano ya sera ya World Governments Summit (WGS), kwa lengo la kubadili majadiliano ya kisera kuwa uwekezaji halisi wenye matokeo ya moja kwa moja katika maendeleo ya nchi za Afrika.

Kupitia ushiriki wake katika jukwaa hilo, Rais Samia anatarajiwa kuendelea kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania katika sekta mbalimbali, ikiwemo nishati, miundombinu, kilimo, utalii na viwanda.

Post a Comment

0 Comments