Tanga Yaimarisha Huduma za Afya kwa Wananchi Wenye Uhitaji

Mkoa wa Tanga unatarajia kuzifikia kaya 51,881 zisizo na uwezo kupitia zoezi la usajili wa Bima ya Afya kwa Wote linalogharamiwa na Serikali, ikiwa ni hatua muhimu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, alipokutana na viongozi wa sekta ya afya mkoani humo kwa ajili ya kujadili maandalizi ya utekelezaji wa zoezi hilo.

Kikao hicho kilihusisha Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Imani Rwatamabanga, Meneja wa NHIF mkoani Tanga, Evance Nyangasi, pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Luluvilo Lulandala.

Dkt. Burian amesema usajili huo utafanyika kwa siku 10 kuanzia Februari 3 hadi 13, 2026, na kuwataka viongozi wa ngazi zote kushirikiana ili kuhakikisha kaya zote zinazostahili zinapatikana na kusajiliwa kwa wakati.

Ameeleza kuwa zoezi hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Afya, Mhe. Omary Nchengelwa, na ni sehemu ya mpango wa siku 100 wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa gharama nafuu.

Aidha, Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za Bima ya Afya kwa Wote, ili kuongeza uelewa na ushiriki wa jamii katika mpango huo.

Ameongeza kuwa maandalizi madhubuti, ushirikiano wa wadau na ufuatiliaji wa karibu ni msingi wa mafanikio ya zoezi hilo.

Post a Comment

0 Comments