Mvutano wa kidiplomasia kati ya Uganda na Marekani unaendelea kuongezeka, kufuatia kauli zilizotolewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kupitia mitandao ya kijamii.
Jenerali Kainerugaba, ambaye pia ni mwana wa Rais Yoweri Museveni, alichapisha ujumbe akidai kuwa Ubalozi wa Marekani mjini Kampala umeingilia masuala ya ndani ya kisiasa ya Uganda. Aidha, alipendekeza kusitishwa kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo operesheni za pamoja za kiusalama katika eneo la Pembe ya Afrika.
Machapisho hayo pia yalimhusu mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine na kuzua mjadala mpana pamoja na mabishano makali mitandaoni. Ndani ya muda mfupi, ujumbe huo ulifutwa.
Baadaye, Jenerali Muhoozi alieleza kuwa taarifa alizozitumia hazikuwa sahihi,na akathibitisha kuwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Uganda na Marekani utaendelea kama kawaida.
Hata hivyo, kauli hiyo haikutosha kutuliza wasiwasi nchini Marekani. Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Seneti ya Marekani, Seneta Jim Risch, alisema kuwa Jenerali Kainerugaba “amevuka mstari mwekundu”.
Seneta huyo alisisitiza kuwa utawala wa Rais Donald Trump unapaswa kutathmini upya ushirikiano wa kiusalama na Uganda, na hata kuzingatia uwezekano wa kuweka vikwazo. Aliongeza kuwa kufutwa kwa ujumbe na kile alichokiita “msamaha usio na maana” hakutosha kurejesha imani.
Kwa upande wake, uongozi wa kijeshi wa Uganda umejibu vikali kauli hizo. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi, Kanali Chris Magezi, alisema matamshi ya seneta huyo ni “mbinu ya kikoloni ya zamani” ya vitisho na kuingilia masuala ya ndani ya nchi, na kusisitiza kuwa Uganda itapinga kwa nguvu mtazamo huo.
Kanali Magezi pia alieleza kuwa ushirikiano kati ya Uganda na Marekani ni wa muda mrefu na unahusisha sekta mbalimbali, hivyo haupaswi kuathiriwa na mabishano ya mitandaoni.
Hadi sasa, Rais wa Marekani Donald Trump bado hajatoa kauli rasmi kuhusu mgogoro huo.
Mvutano huu unajitokeza katika kipindi kinachofuatia uchaguzi wa hivi karibuni nchini Uganda, ambapo Rais Yoweri Museveni alishinda muhula wa saba wa miaka mitano, na hivyo kufikisha takribani miaka 40 madarakani.
Hata hivyo, mpinzani wake mkuu, Bobi Wine, amekataa matokeo ya uchaguzi huo akidai kuwa kulikuwa na dosari na udanganyifu, madai ambayo Serikali ya Uganda imeyakanusha.

0 Comments