Jeshi la Nigeria limesema kuwa vikosi vyake vimefanikiwa kumuua kamanda wa kundi la kigaidi la Boko Haram pamoja na wapiganaji wengine 10, katika operesheni iliyofanyika kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, operesheni hiyo ilifanyika siku ya Jumapili katika msitu wa Sambisa uliopo jimbo la Borno.
Kamanda aliyeuawa ametajwa kuwa Abu Khalid, aliyekuwa wa pili kwa ngazi ya uongozi wa Boko Haram katika eneo la Sambisa. Alielezwa kuwa mtu muhimu ndani ya kundi hilo, mwenye jukumu la kuratibu mashambulizi na mipango ya kigaidi katika eneo hilo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa hakuna mwanajeshi wa Nigeria aliyepoteza maisha wakati wa operesheni hiyo, na kusisitiza kuwa oparesheni za kupambana na ugaidi zinaendelea katika maeneo ya misitu kote kaskazini mashariki mwa nchi.
Boko Haram imekuwa ikitekeleza mashambulizi nchini Nigeria tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, huku maelfu ya watu wakiuawa tangu mwaka 2009.
Tangu mwaka 2015, kundi hilo limepanua mashambulizi yake hadi katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 2,000 katika eneo la Ziwa Chad, kwa mujibu wa mamlaka.
Aidha, maelfu ya wananchi wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi na mapigano yanayoendelea katika eneo hilo.

0 Comments