Mahakama Tanga Kupata Msukumo Mpya wa Huduma Kidijitali

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na Mahakama Kuu Kanda ya Tanga katika kuboresha huduma za kimahakama,ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usikilizaji wa mashauri.

Amesema ushirikiano huo utahusisha pia upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya mahakama na ofisi zake, ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mhe. Balozi Dkt. Batilda ameyasema hayo leo Februari 2, 2026, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika mkoani Tanga, yenye kauli mbiu, “Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa.”

Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na Mahakama utaendelea kuimarika bila kuathiri misingi ya uhuru wa mihimili ya dola.

Amesema maadhimisho hayo yanaonesha dhamira ya Tanzania katika kuimarisha utawala wa sheria kwa mujibu wa Katiba.

Aidha, amesema Mahakama ina nafasi kubwa katika kuleta maendeleo kupitia utatuzi wa migogoro mbalimbali, hususan ya ardhi, jambo linalowezesha wananchi kupata haki kwa wakati.

Kwa mujibu wake, kuongezeka kwa thamani ya ardhi na uelewa wa wananchi kuhusu rasilimali hiyo, ni miongoni mwa sababu zinazosababisha migogoro mkoani humo.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Saidi Johari, ameipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025, ikiwemo kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi.

Amesema hatua hizo zitasaidia kujenga maridhiano, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amesema TLS itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wote katika kutafuta suluhu za kudumu kwa maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments