MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imehitimisha mafunzo ya kijeshi kwa Askari wapya 256 katika hafla iliyofanyika leo Februari 2, 2026, katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amewataka wahitimu hao kuwa wazalendo, waadilifu na watiifu katika kulinda rasilimali za wanyamapori kwa kuzingatia sheria na misingi ya haki.
Amesema Serikali ina imani kuwa mafunzo waliyopewa yatawawezesha kuongeza ufanisi katika kazi za uhifadhi na utoaji wa huduma kwa wananchi bila ubaguzi wa jinsia, dini au kabila.
Aidha, amewahimiza Askari hao kushirikiana na jamii zinazozunguka hifadhi ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za wanyamapori na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Dkt. Abbasi ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuweka sera, mikakati na miongozo madhubuti kwa ajili ya kuimarisha Jeshi la Uhifadhi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amiri Mkalipa, amewataka wahitimu kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali (Mst) Hamis Semfuko, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha ajira ya Askari hao, hatua itakayosaidia kuimarisha uhifadhi na utalii.
Amesema Askari wapya watatumika kikamilifu kulinda rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Awali, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Yussuf Kabange, aliwapongeza wahitimu hao na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa weledi na nidhamu ya kijeshi.


0 Comments