Kalamu za Wahariri Zaitwa Kuokoa Afya ya Taifa

 

WAZIRI wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka wahariri wa vyombo vya habari kutumia nafasi yao kuondoa hofu na upotoshaji miongoni mwa wananchi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, ili waweze kunufaika kikamilifu na huduma za afya.

Amesema hayo leo Februari 2, 2026, wakati wa kikao kazi na wahariri kilichofanyika katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Amesema wahariri wana wajibu mkubwa wa kubadilisha hofu ya wananchi kuwa uelewa sahihi kupitia taarifa zenye ukweli na uwazi.

“Hofu huzaa hasira, na hasira huzaa mgawanyiko. Sauti zenu ni dira, na kalamu zenu ni mwanga utakao waongoza wananchi kesho,” amesema Waziri Mchengerwa.

Ameongeza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kutoa elimu sahihi kuhusu mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, ili kuondoa upotoshaji na kuongeza uelewa wa huduma zitakazotolewa.

Aidha, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, hususan katika kuhudumia makundi maalum pamoja na wagonjwa wa magonjwa sugu.

Ameeleza kuwa wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, atazindua pia mpango maalum wa matibabu kwa wasiokuwa na uwezo, wakiwemo wazee na makundi maalum.

“Mhe. Rais atakapozindua Bima ya Afya kwa Wote, atazindua pia mpango wa kuwahudumia wasiojiweza, hasa katika matibabu ya magonjwa sugu. Wizara imejipanga na iko tayari kutekeleza mpango huo,” amesema.

Post a Comment

0 Comments