Jaji Katarina Mteule Asisitiza Mageuzi ya Kidijitali Mahakamani

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Mteule, amesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yameleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa haki kwa kudhibiti vitendo vya rushwa na ukiritimba mahakamani.

Amesema hayo leo Februari 2, 2026, wakati akihutubia Maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika mkoani Tanga.

Ameeleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yamepunguza kwa kiasi kikubwa ulazima wa wateja kuonana ana kwa ana na watoa huduma, hali inayosaidia kudhibiti vitendo visivyo vya kimaadili miongoni mwa baadhi ya watumishi.

Kwa mujibu wake, maboresho ya TEHAMA yamesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kusikiliza mashauri, ambapo kwa sasa mashauri katika Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya husikilizwa kwa muda usiozidi miezi sita, huku Mahakama ya Mwanzo ikichukua takribani miezi mitatu, tofauti na awali ambapo mashauri yalichukua hadi miaka minne kukamilika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amerejea kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema, “Mchango wa Mahakama katika Ustawi wa Maendeleo ya Taifa,” na kusisitiza kuwa mhimili wa Mahakama una mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo kupitia utatuzi wa migogoro kwa wakati.

Amesema hali hiyo huwasaidia wadaawa kupata haki kwa wakati na kuwawezesha kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Saidi Johari, amesema kauli mbiu ya mwaka huu inaakisi nafasi ya kipekee ya Mahakama katika kulinda haki, kudumisha amani na kuweka mazingira wezeshi ya kisheria, kimuundo na kitaasisi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hotuba yake iliwasilishwa kwa niaba yake na Mwanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Mkoa wa Tanga, Wakili Rebecca Msalangi.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, kupitia hotuba iliyosomwa na Mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Tanga, Wakili Mary Swai, amesema maadhimisho hayo yanakumbusha umuhimu wa utawala wa sheria na Mahakama huru katika kufanikisha maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments