Wakulima Wanufaika na Mpango wa Matrekta 10,000

Serikali imepanga kununua matrekta 10,000 na kuanzisha vituo jumuishi 1,000 vya huduma za zana za kilimo katika ngazi ya Kata, kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za kilimo na kuboresha maisha ya wakulima nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Jumanne, Februari 3, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Kikanda wa Afrika wa Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo uliofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana.

Amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa na rafiki kwa mazingira.

“Kupitia mpango huu, tunalenga kupunguza mzigo wa kazi kwa wakulima, kuongeza tija, kupunguza upotevu wa mazao na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dkt. Mwigulu.

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika zana zinazohimili ukame, mabadiliko ya misimu na athari nyingine za tabianchi ili kulinda usalama wa chakula na kipato cha wakulima.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kushirikisha Sekta Binafsi katika uzalishaji, usambazaji na utoaji wa huduma za zana za kilimo ili kuongeza upatikanaji wake kwa bei nafuu.

“Sekta Binafsi ina nafasi kubwa katika kuharakisha upatikanaji wa zana za kilimo, na Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji,” ameongeza.

Katika kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wengi, Waziri Mkuu amesema vijana na wanawake watawezeshwa kushiriki katika biashara, ubunifu na utoaji wa huduma za zana za kilimo.

Amefafanua kuwa makundi hayo yatapatiwa mafunzo, mitaji na teknolojia ili yaweze kujiajiri na kuajiri wengine.

Kwa mujibu wa Dkt. Mwigulu, mkutano huo umezikutanisha nchi za Afrika kwa kushirikiana na FAO, Umoja wa Afrika, taasisi za fedha, watafiti na wadau wa maendeleo, kwa lengo la kujenga mifumo imara ya huduma za zana za kilimo inayokidhi mahitaji ya wakulima wadogo na wa kati.

Amesema kupitia ushirikiano huo, nchi za Afrika zitaboresha uratibu wa sera, kubadilishana uzoefu na kuendeleza mbinu bora za matumizi endelevu ya zana za kilimo.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Godfrey Chongolo, amesema Serikali itazindua Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo Awamu ya Pili (2026–2035), unaolenga kuimarisha matumizi na utengenezaji wa teknolojia za kisasa katika sekta ya kilimo.

Amesema mkakati huo utaongeza ufanisi katika uzalishaji, uongezaji wa thamani wa mazao na kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Post a Comment

0 Comments