Wadau wa sekta ya kinga ya jamii kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanatarajiwa kukutana jijini Arusha katika mkutano wa kitaifa utakaowakutanisha zaidi ya washiriki 1,200, kwa lengo la kujadili mustakabali wa mifumo ya ustawi wa wananchi nchini.
Mkutano huo utafanyika Februari 9, 2026 katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), na unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kuweka mikakati ya pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya kijamii.
Moja ya matukio makuu katika mkutano huo ni uzinduzi rasmi wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023, inayolenga kuimarisha usalama wa kipato, huduma za kijamii na ulinzi wa makundi yenye uhitaji maalum nchini.
Sera hiyo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na mifumo ya kinga ya jamii kwa mujibu wa kauli mbiu ya “Kinga ya Jamii kwa Wote, Msingi wa Maendeleo.”
Mkutano huo umeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kwa kushirikiana na mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF, PSSSF na WCF, huku ukishirikisha viongozi waandamizi wa serikali, watunga sera, wataalamu wa maendeleo na wadau wa kijamii.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Revocatus Kasimba, amesema mkutano huo ni fursa muhimu ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho katika sekta ya kinga ya jamii.
Kasimba amesema kuwa ushiriki wa viongozi wa ngazi za juu unaonesha dhamira ya serikali katika kuimarisha mifumo ya ulinzi wa wananchi dhidi ya changamoto za kiuchumi na kijamii.
Ameongeza kuwa mkutano huo pia utajadili namna ya kuongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa huduma za hifadhi ya jamii, hususan kwa wananchi wa kipato cha chini na makundi yaliyo hatarini.
Kwa mujibu wa waandaaji, matokeo ya mkutano huo yanatarajiwa kusaidia kuharakisha utekelezaji wa sera na programu za kinga ya jamii, ili kuchangia katika kupunguza umaskini na kuongeza ustawi wa wananchi nchini.


0 Comments