*********
Rais wa Marekani Joe Biden amemuambia Kiongozi wa Urusi Vladmir Putin kwamba kuivamia Ukraine huenda kukababisha mateso mengi ya kibinadamu na kwamba mataifa ya Magharibi yamejitolea katika diplomasia kumaliza mgogoro huo lakini pia yako tayari kwa matukio mengine.
Haya ni kwa mujibu wa ikulu ya Marekani, White House. Hata hivyo, haikutoa pendekezo lolote kwamba mazungumzo hayo ya simu ya saa moja yataondoa tishio la vita barani Ulaya.
Ikulu ya White House pia imemnukuu Biden akisema kwamba Marekani na washirika wake watajibu kwa hatua kali iwapo Urusi itaivamia Ukraine.
Marais hao wawili walizungumza siku moja baada ya mshauri wa Biden wa usalama wa kitaifa Jake Sullivan, kuonya kuwa ripoti ya ujasusi ya Marekani inaonesha kuwa uvamizi wa Urusi huenda ukaanza siku chache zijazo na kabla ya kumalizika Michezo ya Olimpiki ya msimu wa Baridi mjini Beijing Februari 20.
0 Comments