Wanahabari Wapewa Mafunzo Maalum ya Kuripoti Masuala ya Mazingira

Wanahabari kutoka mikoa mbalimbali nchini wameanza mafunzo maalum ya uandishi wa habari za mazingira na uchunguzi, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuripoti kwa weledi masuala yanayohusu uhifadhi wa mazingira na haki za jamii.

Mafunzo hayo, yaliyoanza Februari 5, 2026 jijini Arusha, yanahusisha wanahabari 35 kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Singida na Dodoma, na yameratibiwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya Kusaidia Jamii za Asili (MAIPAC), kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Programu na Uendeshaji wa THRDC, Wakili Halima Sonda, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wanahabari kuchunguza na kuandika kwa kina kuhusu changamoto za mazingira, ikiwemo uchafuzi wa mazingira, ukataji miti, uchimbaji holela wa madini na uharibifu wa vyanzo vya maji.

Amesema kupitia uandishi wa kitaaluma, wanahabari wana nafasi kubwa ya kuibua changamoto zinazowakabili wananchi na kuchochea uwajibikaji wa wahusika wa uhifadhi wa mazingira.

Naye Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, amesema mafunzo hayo yanazingatia pia masuala ya haki za binadamu, hasa kwa jamii za asili zinazotegemea rasilimali za mazingira kwa maisha yao ya kila siku.

Ameeleza kuwa mradi huo unalenga kuwafikia wanahabari zaidi ya 140 nchi nzima, ili kuongeza idadi ya waandishi wenye uwezo wa kuripoti kwa kina masuala ya tabianchi, taka ngumu, uhifadhi wa wanyamapori na matumizi endelevu ya ardhi.

Kwa upande wake, Wakili Paulo Kisabo amesema ni muhimu kwa wanahabari kufahamu sheria zinazohusu mazingira, ardhi na habari, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na bila kukiuka misingi ya kisheria.

Amesisitiza kuwa sheria zilizopo zinawalinda wanahabari wanapotekeleza kazi zao kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma.

Mafunzo hayo yanaendelea jijini Arusha na yanatarajiwa kufanyika pia katika kanda nyingine nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uandishi wa habari za mazingira na kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi wa mazingira.

Post a Comment

0 Comments