Wanawake Watakiwa Kuongoza Ajenda ya Usawa wa Kijinsia katika Uchumi wa Buluu


Tanga:
Kongamano la usawa wa kijinsia katika mabadiliko ya tabianchi limefanyika mkoani Tanga, likiwa na lengo la kujadili nafasi ya wanawake katika kuchagiza maendeleo ya uchumi wa buluu na ushiriki wao katika maamuzi muhimu ya kisera.

Akizungumza katika kongamano hilo Msimamizi Mkuu wa Mradi Kikanda wa ReSea,Ms Perpetual Angima,amesema wanawake ni sehemu muhimu ya uchumi wa buluu lakini bado hawapati nafasi za kutosha katika ngazi za maamuzi,hali inayowafanya kukosa wawakilishi wa kuwatetea.

Ameeleza kuwa tathmini ya sera imebaini uwepo wa mapungufu katika utekelezaji wake, akisisitiza kuwa ni muhimu sera hizo zisibaki kwenye maandishi bali zibadilishwe na kuwekwa katika vitendo ili kuleta usawa wa kweli wa kijinsia.

Ms.Angima amesema kuna umuhimu wa kuboresha mifumo iliyopo ili kuhakikisha wanawake wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kupanga na kusimamia shughuli za uchumi wa buluu, ikiwemo uvuvi na uhifadhi wa rasilimali za bahari.
Aidha,amesisitiza haja ya kubadili dhana ya ushirika kutoka kuwa ya kawaida na kuifanya kuwa chombo cha ushawishi, akieleza kuwa wanawake wakipewa nafasi huonyesha uwezo mkubwa katika usimamizi wa rasilimali.

Kwa upande mwingine, amesema mradi wa ReSea umejikita katika kuwekeza katika uongozi wa wanawake na vijana kwa lengo la kuongeza ushiriki wao katika uchumi wa buluu na kuhakikisha wanakuwa sehemu ya mabadiliko ya sera.

Ameongeza kuwa mradi huo unatumia ushahidi katika kufuatilia utekelezaji wa usawa na ujumuishaji, ili kuhakikisha kuwa hatua zinazochukuliwa zina matokeo chanya kwa jamii.
Washiriki wa kongamano hilo wameeleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaathiri zaidi wanawake, hivyo kuna haja ya kuwawezesha kwa kuwapa elimu,rasilimali na fursa za kiuchumi ili kukabiliana na changamoto hizo.

Kongamano hilo lilikuwa na kaulimbiu isemayo: “Kuendeleza Uchumi wa Buluu unaozingatia usawa, haki na maendeleo shirikishi kwa ustawi wa mazingira.”

Post a Comment

0 Comments