Mahakama Kuu ya Abuja nchini Nigeria imewahukumu wanaume wanne kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya ugaidi kuhusiana na shambulio la mwaka 2022 katika Kanisa Katoliki la St. Francis Xavier lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 40.
Jaji Emeka Nwite alitoa hukumu hiyo siku ya Jumatano baada ya kuwatia hatiani Idris Abdulmalik Omeiza, Al Qasim Idris, Jamiu Abdulmalik na Abdulhaleem Idris kwa makosa tisa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupinga Ugaidi ya mwaka 2022.
Makosa hayo yanajumuisha kujiunga na kundi la kigaidi, kupanga njama na kutekeleza mauaji yaliyotokea katika mji wa Owo, Jimbo la Ondo, kusini-magharibi mwa Nigeria.
Shambulio hilo lilihusisha kufyatua risasi na kurusha mabomu ndani ya Kanisa Katoliki la St. Francis Xavier, ambapo zaidi ya watu 40 waliuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa.
Mahakama ilimhukumu kila mmoja kifungo cha maisha jela, huku mshtakiwa wa tano, Momoh Otuho Abubakar, akiachiliwa huru baada ya kutopatikana na hatia.
Akizungumza baada ya hukumu hiyo, mwendesha mashtaka Ayodeji Adedipe alisema haki imetendeka kwa waathirika na familia zao.
Hata hivyo, wakili wa washtakiwa, Abdullahi Muhammad, amesema upande wa utetezi haujaridhika na uamuzi huo na unapanga kukata rufaa mahakamani.

0 Comments