Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, amesema maazimio yote yaliyopitishwa kwenye mkutano mkuu wa kimataifa wa mabaraza ya habari Afrika na duniani, uliofanyika mkoani Arusha, yapo manne na ni muhimu yazingatiwe kwani yanagusa mwelekeo wa mafunzo waliyonayo.
Sungura ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu kupambana na taarifa potofu, upotoshaji na habari za chuki wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, yanayofanyika Millennium Tower, Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Amesema, katika mkutano huo walipitisha azimio moja la msingi sana, ambalo ni serikali za mataifa ya Afrika ziwekeze kwa kiasi kikubwa katika teknolojia na uchumi wa kidigitali. Amesisitiza kuwa azimio hilo la msingi linapaswa kufikishwa kwenye kila wizara husika na kila taifa, kwani limepitishwa na wadau walioshiriki kwenye mkutano huo na hivyo serikali za mataifa husika zitalazimika kulizingatia.
Ametaja azimio la pili kuwa ni serikali za mataifa ya Afrika kutunga sheria, kanuni na sera zinazozingatia ukuaji wa matumizi ya teknolojia na akili bandia.
“Kukua kwa matumizi ya teknolojia na kuweka mazingira wezeshi kwa taaluma ya habari kutatekeleza wajibu wake. Vyombo vya habari vina wajibu wa kutambua majukumu yao, lakini wanahitaji mazingira wezeshi yanayoundwa na sheria, sera, kanuni na taratibu. Hivyo, wamepitisha azimio la kuyataka mataifa ya Afrika kutunga sheria na kanuni zinazotengeneza mazingira hayo wezeshi,” amesema.
Ametaja azimio la tatu kuwa ni mataifa ya Afrika kulinda utamaduni wa Kiafrika na kutunza kumbukumbu ya urithi wa namna habari za Afrika zinavyopaswa kusimuliwa, kwa kuepuka kuchakachuliwa na utamaduni wa kigeni.
“Sasa hivi dunia imehamia mtandaoni, na huko mtandaoni kuna utamaduni wa kigeni unaotamalaki. Azimio hili lililenga tuzingatie utamaduni wetu na namna tunavyosimulia simulizi na urithi wa Kiafrika kwa faida ya Afrika. Na sisi lazima tuendelee kulinda namna tunavyosimulia habari za Afrika kwa faida ya Waafrika wenyewe,” amesema.
Amesema azimio la nne ni kuhusu vyuo vya uandishi wa habari na vyuo vikuu, kwani vijana wa leo walioko vyuoni wanaweza kuwa mbele zaidi kiteknolojia kuliko walimu wao. Ameeleza kuwa inapaswa kuandaliwa mitaala inayowawezesha walimu kuwa na ufahamu na upeo mkubwa wa masuala ya kiteknolojia na akili bandia, pamoja na mitaala inayokidhi mahitaji yanayoendana na teknolojia na kuzingatia matumizi ya akili bandia.
Amefafanua kuwa anashukuru vyombo vya habari kwa ushirikiano wao katika kufanikisha mkutano mkubwa wa kimataifa uliofanyika mkoani Arusha.
Amesema Tanzania inapaswa kuwa ofisi ndogo ya Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani, kwani ni mara ya kwanza tangu umoja huo uanze miaka 40 iliyopita, kutoka Afrika na hasa Tanzania.
“Kutokana na hilo, kuna pendekezo la kuifanya Tanzania kuwa sub-head office, ili Katibu Mkuu anapotokea aweze kuona namna utekelezaji wa mambo unavyokwenda vizuri,” amesema.
“Tunataka tuonekane tunatangaza mambo ya kimataifa, na dunia yote ijue. Vyombo vyote vya habari vibebe hiyo ajenda. Tukamate hizo ajenda, tuzipeleke kwenye kila baraza la habari kote Afrika na nje ya Afrika. Naomba ushirikiano ambao mmeutoa tuendelee kuutumia vizuri katika nafasi hii,” ameongeza.
“Sisi wenyewe, Baraza la Habari Tanzania, tunahitaji kujielimisha. Kwa azimio kama hili, inatakiwa mitaala ya elimu katika vyuo izingatie masuala ya kiteknolojia na akili bandia, ikitamka wazi faida zake na namna production inaweza kufanyika kwa kutumia akili bandia, na pia kueleza madhara yake ili watu wajue,” amesema.
0 Comments