Serikali ya Burkina Faso imetangaza kuchukua hatua za uwiano kufuatia kuingizwa kwa nchi hiyo katika orodha ya marufuku kamili ya kusafiri kwenda Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne na Wizara ya Mambo ya Nje ya Burkina Faso, serikali imesema itaweka masharti sawa ya utoaji wa viza kwa raia wa Marekani, ikieleza kuwa hatua hiyo inazingatia kanuni ya uwiano katika mahusiano ya kimataifa.
“Serikali ya Burkina Faso inaendelea kujitolea kuheshimu misingi ya heshima ya pande zote, usawa wa nchi huru na kanuni ya uwiano katika uhusiano wake wa kimataifa,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo ilisisitiza kuwa Burkina Faso inaendelea kuwa wazi kwa ushirikiano wa kimataifa unaojengwa juu ya kuheshimiana kwa maslahi ya pande zote, bila kujali hatua zilizochukuliwa na washirika wake.
Hatua kama hiyo pia imechukuliwa na mataifa ya Mali na Niger, ambayo nayo yameathiriwa na marufuku ya kusafiri iliyotangazwa na Marekani.
Kupitia taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Mali ilisema kuwa, kuanzia mara moja, raia wa Marekani watatakiwa kutimiza masharti na vigezo vya viza vinavyofanana na vile vinavyowekwa kwa raia wa Mali wanaotaka kuingia Marekani.
“Kwa mujibu wa kanuni ya uwiano, Serikali ya Jamhuri ya Mali itaweka mahitaji sawa ya viza kwa raia wa Marekani,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza vikwazo vipya vya kusafiri vinavyohusisha marufuku kamili au ya sehemu kwa raia wa nchi 39, nyingi zikiwa barani Afrika.
Uamuzi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi tarehe 1 Januari 2026, na unalenga kuzuia au kupunguza kwa kiwango kikubwa uingiaji wa raia kutoka nchi zilizoathiriwa kuingia nchini Marekani.

0 Comments