Mkuu wa Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Japhari Kubecha, ameisifu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Gairo kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika ukusanyaji wa mapato ya serikali, akieleza kuwa mapato hayo yamekuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani humo.
DC Kubecha alitoa pongezi hizo alipokutana ofisini kwake na Meneja wa TRA Wilaya ya Gairo, Ditram Wila, pamoja na Afisa Mwandamizi wa Elimu na Mawasiliano wa TRA Mkoa wa Morogoro, Immaculate Chaggu, waliomtembelea kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikazi.
Katika kikao hicho, DC Kubecha alipokea zawadi ya Ushirikiano wa Mwaka 2025 kutoka TRA, kama ishara ya kutambua mchango wake katika kuhamasisha ulipaji wa kodi na kuimarisha mshikamano kati ya mamlaka hiyo, viongozi wa serikali na wafanyabiashara.
Alisema mafanikio yanayoonekana katika ukusanyaji wa mapato yanatokana na ushirikiano wa karibu kati ya TRA na wadau wake, hususan wafanyabiashara, akibainisha kuwa mazingira ya uwazi na haki yameongeza uaminifu na hiari ya walipakodi kutimiza wajibu wao kwa wakati.
Wafanyabiashara wa Wilaya ya Gairo nao wameeleza kuridhishwa na namna TRA inavyotoa elimu ya kodi pamoja na huduma rafiki, wakisema hatua hiyo imepunguza sintofahamu katika masuala ya kodi na kusaidia ukuaji wa shughuli zao za kibiashara.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Wilaya ya Gairo, Ditram Wila, alisema mamlaka hiyo itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa kuzingatia sheria na kutoa huduma bora kwa walipakodi, ikiwa ni pamoja na kuwafuata wafanyabiashara moja kwa moja katika maeneo yao ili kufanya tathmini sahihi ya kodi.
Aliongeza kuwa TRA imekuwa ikifanya ziara katika minada, masoko na vituo vya biashara wilayani Gairo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati na kutoa risiti halali kwa wateja.
Katika ziara hizo, TRA ilitoa pia zawadi kwa baadhi ya wafanyabiashara na viongozi wa wilaya, akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Gairo, Jeremia Mapogo, kama sehemu ya kuendeleza ushirikiano na kutambua mchango wao katika kukuza mapato ya serikali.
0 Comments