SERIKALI YAAGIZA KUHARAKISHWA KWA MRADI WA BWAWA LA MAJI KIDUNDA

WAZIRI MKUU Dkt.Mwigulu Nchemba ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha kuwa mradi wa Bwawa la Maji Kidunda haukwami na unakamilika kwa wakati ili uanze kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Ameyasema hayo leo Ijumaa, Januari 2, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo lililopo Wilaya ya Morogoro, mkoani Morogoro.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Dkt. Mwigulu amesema mradi wa Bwawa la Kidunda unaakisi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi.

“Kiongozi wetu ana maono ya mbali; aliamua kuutekeleza mradi huu katika kipindi ambacho Serikali ilikuwa pia ikitekeleza miradi mingine mikubwa na ya kimkakati inayohitaji fedha nyingi. Hii inaonesha dhamira ya Serikali ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili Watanzania,” amesema Dkt. Mwigulu.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Maji kuandaa jedwali la utekelezaji litakalomsaidia mkandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema kukamilika kwa mradi huo unaogharimu takribani shilingi bilioni 366 kutasaidia kuzalisha karibu megawati 20 za umeme. Amesema pia, mbali na kutoa huduma ya maji, mradi huo utawezesha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 72.

Ameongeza kuwa bwawa hilo litawezesha kuhifadhi takribani lita bilioni 190 za maji, yatakayosaidia matumizi ya majumbani hususan wakati wa kiangazi pale kina cha Mto Ruvu kinapopungua.

Naye Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya kilimo, akieleza kuwa maeneo yanayozunguka bwawa hilo yanafaa kwa shughuli za kilimo. Amebainisha kuwa Wizara ya Kilimo itawezesha utekelezaji wa kilimo cha umwagiliaji katika maeneo hayo.

Post a Comment

0 Comments