Ebo Noah:Nabii aliyedai kutabiri mwisho wa dunia siku ya Krismasi akamatwa

Nabii anayejiita mwenyewe Ebo Noah pichani,anaripotiwa kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi la Ghana katika mkesha wa Mwaka Mpya. Kukamatwa kwake kunakuja siku chache baada ya utabiri wake uliosambaa duniani kote kwamba dunia ingeisha siku ya Krismasi.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, kukamatwa kwa Noah kulifanyika chini ya maagizo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspector General of Police), kupitia kikosi maalum cha utekelezaji wa sheria. Taarifa zinaeleza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa baada ya utabiri wake kuzua taharuki kubwa, huku watu wengi wakimfuata hadi kwenye safina (arks) alizojenga.

Nabii huyo wa Ghana, ambaye jina lake halisi ni Evans Eshun, alivuta hisia za watu duniani baada ya kudai kuwa alipokea maono kutoka kwa Mungu yaliyomweleza kuwa dunia ingeangamia siku ya Krismasi mwaka 2025, kufuatia mafuriko makubwa.

Katika maandalizi ya tukio hilo alilodai kutokea, Ebo Noah alijenga safina mbili kubwa, akiwakaribisha wote waliotaka kuokoka dhidi ya mafuriko hayo kujiunga naye. Hata hivyo, baada ya Krismasi kupita bila tukio lolote la mafuriko au mwisho wa dunia, mamlaka zilianza kuchukua hatua dhidi yake.

Jeshi la Polisi la Ghana bado halijatoa maelezo ya kina kuhusu mashtaka yanayomkabili, huku uchunguzi ukiendelea.

Post a Comment

0 Comments