Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA (T) Musa Nassoro Kuji, pamoja na bingwa wa dunia wa mbio ndefu za mwaka 2025, Alphonce Simbu, jana Desemba 31, 2025 walipokelewa kwa heshima kubwa Zanzibar kufuatia mwaliko maalum kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwaliko huo ulihusisha ushiriki wa TANAPA na bingwa huyo wa dunia katika Bonanza Maalum la Mazoezi ya Viungo Zanzibar 2026, lililofanyika asubuhi ya leo Januari 1, 2026, likianza kwa matembezi ya pamoja.
Matembezi hayo yaliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, yakianzia eneo la Michenzani hadi Uwanja wa New Amani Complex, uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Katika kuhitimisha bonanza hilo, bingwa wa dunia wa mbio ndefu Alphonce Simbu alitambulishwa rasmi kwa washiriki wa mazoezi hayo, ambapo pia alipata fursa ya kupiga picha ya kumbukumbu na Mhe. Rais wa Zanzibar.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa bonanza hilo, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA (T) Musa Nassoro Kuji, alimshukuru Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaliko huo maalum, akisema kuwa ushiriki wa TANAPA pamoja na mwanariadha huyo wa kimataifa utatoa hamasa kwa vijana wanariadha wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kamishna Kuji alisema kuwa ujio wa Alphonce Simbu ni chachu kwa vijana kuweka nia na bidii katika michezo, hususan riadha, ili kufikia viwango vya kimataifa kama alivyo Simbu.
“Kipekee ninamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna anavyoipa kipaumbele sekta ya utalii na michezo nchini. Jitihada hizi zimechangia kukuza vipaji vya wanamichezo wanaofanya vizuri kimataifa, akiwemo Alphonce Simbu,” alisema Kamishna Kuji.
Aliongeza kuwa anamshukuru pia Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa mwaliko huo maalum uliowezesha TANAPA kushiriki bonanza hilo kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

0 Comments