Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imesisitiza umuhimu wa kufanyiwa marekebisho ya haraka kwa Sera na Sheria ya Huduma za Habari ili ziendane na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya kidijitali na mitandao ya kijamii nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo ameeleza kuwa sheria iliyotungwa mwaka 2016 haikutazama kwa upana mchango wa bloga na watengeneza maudhui ya mtandaoni,ambao kwa sasa wamekuwa sehemu muhimu ya tasnia ya habari.hivyo mapitio hayo yanakusudia kuwajumuisha rasmi katika mfumo wa kisheria na usimamizi wa kitaaluma.
Akitoa wasilisho katika mkutano wa mwaka wa utangazaji 2026 uliofanyika Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Patrick Kipangula, alisema kuwa mfumo wa ithibati umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, kwa lengo la kulinda maslahi ya umma, kukuza maadili, na kuimarisha uwajibikaji katika taaluma ya uandishi wa habari.
Ameeleza kuwa JAB kwa sasa inatekeleza jukumu la kutoa ithibati kupitia mfumo wa kidijitali wa TAI-HABARI, unaowawezesha waandishi waliokidhi vigezo kupata vitambulisho vya kazi (Press Cards) vinavyodumu kwa miaka miwili. Takwimu zinaonesha kuwa hadi Januari 2026, zaidi ya maombi 3,200 yalikuwa yameidhinishwa, huku mengine yakiendelea kufanyiwa tathmini.
Hata hivyo, Bodi imebainisha changamoto ya baadhi ya wadau kuwa na mtazamo potofu kuhusu ithibati, wakidhani ni njia ya kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari badala ya chombo cha kuimarisha ubora na uaminifu wa kazi za uandishi.
Pia imeelezwa kuwa uelewa mdogo wa matakwa ya sheria unasababisha baadhi ya waandishi kuwasilisha maombi yasiyokidhi vigezo, ikiwemo hitaji la kuwa na angalau Stashahada au Shahada ya Uandishi wa Habari. JAB imeonya kuwa kufanya kazi bila ithibati halali ni kinyume cha sheria na kunaweza kusababisha hatua za kinidhamu.
Kwa mujibu wa Wakili Kipangula, Bodi itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na taasisi za mafunzo ya uandishi wa habari ili kuongeza uelewa wa sheria na kuhakikisha mfumo wa ithibati unalinda maslahi ya waandishi na jamii kwa ujumla kupitia utoaji wa habari sahihi na zenye weledi.
.jpeg)
0 Comments