Tunisia imebadilisha adhabu kwa watu wanaosambaza taarifa za kupotosha mitandaoni, ambapo sasa watakaobainika kufanya makosa hayo watatozwa faini badala ya kufungwa jela.
Marekebisho hayo yanaweka faini kati ya dinari 10,000 na 20,000 za Tunisia, sawa na dola za Marekani 3,300 hadi 6,600.
Sheria hiyo pia inawahusu wanaosambaza nyaraka za uongo au za kupotosha, taarifa binafsi za watu au madai ya uongo yanayoweza kuharibu sifa, heshima na utu wa mtu.
Hata hivyo, mtu atakayekutwa akirudia kosa anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miezi sita jela pamoja na faini ya dinari 50,000, sawa na zaidi ya dola 16,000.
Adhabu hizo zinaweza kuongezwa mara mbili iwapo kosa litafanywa na mtumishi wa umma au mtu mwenye nafasi kama hiyo.
Marekebisho hayo yamefanyika baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais Kais Saied, kilichojadili mabadiliko ya Kifungu cha 54 na sheria nyingine.
Kifungu hicho kimekuwa kikikosolewa na mashirika ya haki za binadamu, yakieleza wasiwasi kuhusu athari zake kwa uhuru wa kujieleza.

0 Comments