TANGA YEMEN SOCIETY WAKABIDHI KISIMA SHULE YA SEKONDARI TANGA TECH




Na Mashaka Mhando, Tanga

TAASISI mpya ya Kiislamu ya Tanga Yemen Society for Charity (TYSC), imezindua kisima chake cha kwanza cha msaada walichokijenga katika shule ya sekondari,Tanga Ufundi.

Taasisi hiyo, inayoendeshwa na Watanzania na watu wa Yemen, imeanzishwa hivi karibuni ikiwa na lengo la kusaidia jamii ikiwemo kutoa elimu ya dini ya kiislamu.

Akizindua kisima hicho, Meya wa Jiji la Tanga, kilichofadhiliwa na Fathhiya Foundation ya Moshi,  Abdulhaman Shilow, alisema halmashauri itawaunga mkono katika jituhada zao za malengo yakusaidia jamii Jijini hapa na Tanga kwa ujumla.

"Baraza la madiwani la Halmashauri ya Jiji, inawaunga mkono katika malengo yenu na inawatia moyo muwe chachu ya kusaidia jamii ya wana-Tanga, " alisema Meya Shilow.

Awali Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Abdallah Said Bazar alisema kisima hicho ni cha kwanza tangu waianzishe taasisi yao baada ya kuombwa na wanafunzi wanaoswali katika msikiti uliopo shuleni hapo.

"Mheshimiwa Mstahiki Meya, kisima hiki ni cha kwanza tangu tuanze kufanya kazi, na huu ni mwanzo bado mipango na malengo yetu ni kusaidia jamii zaidi katika miradi ya maendeleo kwa jamii yetu, " alisema Mwenyekiti huyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Ahmed Basalama, alisema taasisi hiyo itajikita zaidi katika kusaidia majanga ya moto, kusaidia vituo vya kulelea watoto yatima pamoja na kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu.

Hata hivyo, alisema taasisi hiyo iliyokuwa na kituo cha kufundisha watoto barabara ya nane, imepanga malengo ya muda mrefu kujenga hospitali na shule.

"Taasisi yetu katika malengo ya baadae tumepanga kujenga hospitali, shule na tutakuwa na kliniki ya masuala mbalimbali kwa watu wenye shida, " aliaema Naibu Katibu huyo na kugusia kwamba hivi karibuni wanatarajia kuanzisha darasa la kufundisha kompyuta.

Mkuu wa shule ya Tanga Ufundi Andrew Mwakanyamale, alishukuru kwa msada wa kuchimbiwa kisima hicho ambacho kitaongeza idadi ya vyanzo vya maji katika jumuiya ya shule hiyo.

Alisema shule hiyo yenye wanafunzi wapatao 1,174, wanahitaji matumizi makubwa ya maji kwa mahitaji ya kila siku na kabla wana matenki ya lita 30 huku maji ya Tanga-Uwasa yakitumika jikoni.

"Uzinduzi wa kisima hiki utatusaidia katika maeneo yetu mengi ya jumuiya ya shule na hasa hapa msikitini na mabweni yaliyokuwa karibu, " alisema mwalimu huyo.

Mwangalizi wa msikiti huo Ahmed Mohamed ambaye ni mwanafunzi katika risala ya shukrani alitoa ombi la kujengewa uzio utakaotenganisha sehemu ya kuswalia waumini wa kike na kiume hasa eneo la choo.

Pia mwangalizi huyo aliomba kupatiwa kipaza sauti ili kitumike katika msikiti huo wakati wa ibada kwa kuwa sasa idadi ya wanafunzi wanaoabudu katika msikiti huo imeongezeka kutoka watu 70 hadi kufikia 405.

Hata hivyo,  mgeni rasmi katika uzinduzi wa kisima hicho Meya Shilow aliwaomba wanafunzi wasiwaze kutumia kipaza sauti katika msikiti wao ili usilete bughudha kwa jamii nyingine badala yake amewashauri siku ya Ijumaa wakaswali katika misikiti mingine iliyopo jirani na shule hiyo.

Post a Comment

0 Comments